Mashahidi 3 kutoa ushahidi dhidi ya mwenyekiti UVCCM mkoa Arusha aliyejifanya Afisa usalama wa Taifa

Na.Vero Ignatus ,Arusha .
 Mashahidi wa watatu, akiwepo afisa usalama wa Taifa, mwandamizi, Editha Aveline watatoa ushahidi katika kesi ya kujifanya usalama wa taifa inayomkabili,  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM(UVCCM) mkoa wa Arusha  ,Lengai  ole Sabaya.

Wakili wa Serikali Riziki Mahanyu ,alitoa taarifa hiyo jana,Mbele ya hakimu mkazi Gwantwa Mwankuga wakati akisoma maelezo ya awali ya kesi ya kujifanya afisa usalama kiongozi huyo wa UVCCM ambaye pia ni Diwani wa kata ya Sambasha.

Mahayu alisema mashahidi wengine katika kesi hiyo, watakuwa ni lnspekta Rogat  pamoja na Meneja wa hoteli   Philipo John.

Alisema Jamhuri  pia itawasilisha Kitambulisho cha kugushi cha Sabaya, kinachodaiwa ni cha usalama na mtuhumiwa ,risiti ya hoteli ya Sky way yenye namba 0983 na hati ya kuchukua mali polisi 

Alisema Sabaya ( 29 ) alitenda makosa hayo Mei 18 mwaka huu, hoteli ya Sky way ,ambako alikaa kwa siku 5 hotelini hapo kwenye vyumba vyenye gharama ya shilingi 30,000 za kitanzania  ,ambako baada ya kuingia hotelini hapo alikabidhi kwa uongozi wa hoteli  simu yake aina ya Samsung pamoja na kitambulisho hicho 

Pia alisema licha ya kukaa siku hizo ,aliondoka bila kutoa taarifa wala kulipa deni la shilingi 309,000 alizokuwa anadaiwa hotelini hapo ,ambako 150,000 ilikuwa ni ya malazi na 159,000 ilikuwa ya vinywaji ,baada ya kukaa  kwa muda mrefu bila kulipa meneja wa hoteli hiyo ,alipeleka  malalamiko hayo kwa balozi na mwenyekiti wa mtaa na ndipo walipomshauri apeleke kesi hiyo polisi 

Aliongeza baada ya kupeleka kesi hiyo polisi ,alitafutwa na kukamatwa lakini baada ya kulipa deni alikabidhiwa simu yake na kitambulisho kilikuwa kipo kituo cha polisi cha kati 

Baada ya kusomewa maelezo ya awali kutoka kwa wakili wa jamhuri ,mwendesha kesi ,hakimu mkazi  Mwankuga ,alimuuliza maswali mshtakiwa huyo kuwa kama jina lake ni sahihi ,kitambulisho ni chake na  kama alikamatwa na polisi 

Mshtakiwa Lengai Sabaya ,alikiri jina ni lake ,na kukiri kuwa kweli alikamatwa na polisi lakini alikana kuhusishwa na hizo tuhuma ikiwemo kitambulisho hicho .

Kesi hiyo, imepangwa  kuanza kusikilizwa Desemba 7 mwaka huu, ambapo kwa mara ya kwanza,Sabaya  septemba 19 alisomewa mashtaka mawili ya kujifanya mtumishi wa umma wa usalama wa taifa pamoja na kugushi kitambulisho cha idara ya usalama wa taifa chini ya kitengo cha kikosi maalum
Powered by Blogger.