Wananchi 700 wilayani Ukerewe hawana pa kuishi baada mvua kuharibu nyumba zao.

Zaidi ya watu 700 katika vijji vitano vya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, hawana makazi baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kuezua mapaa ya nyumba zao 118,kuharibu migomba na mazao mengine ya chakula mashambani pamoja na miundombinu ya umeme,huku kamati ya maafa wilayani humo ikiomba msaada wa haraka kutoka kwa watu mbalimbali wa ndani na nje ya wilaya hiyo.

Kamati ya maafa ya wilaya ya Ukerewe,ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Estomii Chang’a, imetembelea katika vijiji vya Bwasa,Igalla,Chankamba,Busiri na Lutare ili kujionea athari za mvua hiyo na kuwapa pole wananchi waliofikwa na maafa hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Frank Bahati anasema tayari Halmashauri yake imetoa msaada wa mabati 200 pamoja na magodoro 20 vyenye thamani ya shilngi miloni nane na laki tisa,lakini bado anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada zaidi ya kibinadamu.

Diwani wa kata ya Igalla Joshua Manumbu,ametoa rai kwa wananchi kuanza kufanya ukarabati wa nyumba zao zilizoezuliwa badala ya kusubiri msaada wa serikali,huku baadhi ya wananchi wakiishukuru serikali wilayani humo kwa hatua ya kuwasaidia mabati na magodoro.

Baadhi ya taasisi za serikali zilizoathirika na mvua hiyo iliyonyesha usiku wa kuamkia jana kwa muda wa saa tatu mfululizo ni pamoja na shule ya msingi Chankamba,ambako nyumba ya mwalimu imeezuliwa paa,sambamba na kuanguka kwa jengo la kigango cha kanisa katoliki Chankamba na kanisa la The last Church of Christ kijijini hapo, ambapo serikali imeahidi kuyasaidia makanisa hayo mabati 30 kila moja.
Powered by Blogger.