Wachimbaji wadogo wa madini walia na mikataba ya wawekezaji

Wachimbaji wadogo wa madini katika kata ya Matundasi wilayani Chunya wakiendelea na utafutaji wa madini aina ya dhahabu.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wilayani Chunya mkoani Mbeya wameiomba serikali kupitia upya mikataba ya madini inayotolewa kwa kampuni za uchimbaji na kutoa kipaumbele kwa wakazi waliopo katika maeneo yenye madini.

Ombi hilo limetolewa na wachimbaji hao katika kijiji cha Itumbi wilayani humo na ambapo wamesema kuwa tangu eneo hilo la wachimbaji wadogo kutolewa kwa wawekezaji wakubwa imefanya wawe na maisha magumu kutokana na kukosa sehemu ya kufanyia shughuli zao.

Wachimbaji hao wamesema kuwa hali hiyo inasababisha wao kwenda kuvamia maeneo ya wawekezaji hao wakubwa ambapo inapelekea wengine kupigwa risasi na kupoteza maisha kutokana na matukio hayo jambo linaloharibu sura ya taifa.

Aidha wananchi hao wamesema kuwa hawaoni faida ya kuwepo kwa makampuni hayo ya uchimbaji madini ya dhahabu kutokana na kukosa ajira kutoka kwa wawekezaji hao kama ambavyo mikataba yao inawaelekeza.

Kwa upande wake mmoja wa wawekezaji wa Kampuni ya Sunshine kutoka nchini China amesema wameshindwa kutoa ajira kwa wakazi wengi zaidi kwa wazawa kutokana na teknolojia wanayotumia kuwa inahitaji elimu zaidi.
Powered by Blogger.