Tanesco yazidi kubanwa kuhusu bei ya umemeWanachi wamepinga azma ya shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupandisha bei ya umeme huku wakisema sababu zilizowasilishwa na shirika hilo hazina mashiko ya kutosha kushawishi bei kupanda.
tanescopic
Hayo yamejiri Jumatano hii jijini Dar es Salaam, wakati wadau na wananchi wa mkoa huo waliojitokeza kutoa maoni yao kwenye mkutano wa taftishi ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ambao ndio wahusika kwa suala hilo.
Wakitoa maoni yao mbele ya Ewura na Tanesco, wadau hao walisema pamoja na shirika hilo kuwasilisha sababu za wao kupendekeza kupandisha bei ya umeme, lakini hazina mashiko ya kutosha kuidhinisha maombi yao.
Kwa upande wao Baraza la Ushauri la Serikali (EWURAGCC), lilisema limefanya uchambuzi wa maombi hayo na kubaini kuwa ni kweli uendeshaji wa shirika hilo una gharama kubwa kuliko fedha zinazopatikana.
Lakini sababu hiyo pamoja na nyingine zilizoainishwa na shirika hilo, hazitoshelezi kushawishi wananchi kukubali kupanda kwa bei ya umeme.
“Tumepitia sababu za Tanesco kuomba kupandisha bei ya umeme, ni kweli tumeona moja ya sababu ni kuwa shirika linaendeshwa kwa gharama kubwa kuliko fedha zinazopatikana, ila pamoja na sababu nyingine, bado hazitoshi kushawishi wananchi kukubali bei kupanda,” alisema Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Amani Mafuru.
Awali Novemba 4, mwaka huu Ewura ilipokea maombi ya Tanesco ya mapendekezo ya kurekebisha bei ya umeme na waliyapitia na yalikidhi vigezo hivyo wakaandaa mikutano ya wadau kutoa maoni yao kuanzia Novemba 16 hadi hiyo jana na kesho watafunga pazia la kupokea maoni.

CHANZO:HABARILEO
Powered by Blogger.