Polisi wamtia nguvuni kipa wa Timu ya Yanga Benno Kakolanya

KIPA WA YANGA, BENNO KAKOLANYA.

KIPA wa Yanga, Benno Kakolanya jana alishindwa kuhudhuria mazoezi ya timu yake kufuatia kukamatwa na askari wa usalama barabarani akiwa amepanda pikipiki bila kuvaa kofia maalum maarudfu kama Helmet.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kwamba Kakolanya ni kati ya wachezaji saba ambao hawakuhudhuria mazoezi Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali.

“Benno Kakolanya alipiga simu kutuambia amekamatwa na trafiki akiwa amepanda pikipiki bila kuvaa Helmet sasa wakati anapiga simu tena baada ya kuachiwa, tulikuwa tumekwishamaliza mazoezi, hivyo hakuja kabisa,”alisema Hafidh.

Mbali na kipa huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Prisons ya Mbeya, wengine ambao hawakufika mazoezini jana ni beki Mtogo Vincent Bossou, kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, washambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, Mzambia, Obrey Chirwa na wazawa beki Hassan Kessy na mshambuliaji Malimi Busungu.

“Bossou ana ruhusa maalum yupo kwao Togo, Ngoma ana matatizo ya kifamilia, Busungu alikuwa anashughulikia kesi yake ya ajali, Kessy naye alikuwa anashughulikia kesi yake na Simba, lakini Niyonzima na Chirwa kwa kweli sina taarifa zao,”alisema.

Hafidh aliwataja wachezaji 18 waliofika mazoezini jana kuwa ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Wengine ni viungo Simon Msuva, Deus Kaseke, Mkongo Mbuyu Twite, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Matheo Anthony.

Kinda Yussuf Mhilu aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana, yupo na kikosi cha U-20 Bukoba mkoani Kagera kwenye Ligi Kuu ya Vijana.

Yanga imeanza mazoezi jana Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam chini ya benchi la jipya lam Ufundi, lililopanuliwa kufuatia ujio wa kocha mpya, Mzambia, Geeorge Lwandamina anayechukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm anayehamia kwenye Ukurugenzi wa Ufundi.

Na Yanga inajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani.
Powered by Blogger.