Mtangazaji wa SuperSport alivyomtangaza Chaila wa ZESCO kuwa anatua Simba

Mmoja wa watangazaji wa Kituo cha Televisheni cha SuperSport juzi aliutangazia umma kuwa kiungo wa Zesco, Misheck Chaila, anakwenda Simba.
Kiungo huyo amekuwa akitajwa kama kati ya viungo mahiri zaidi kwenye kikosi hicho cha Zesco ambacho kilifanya vizuri kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kuondolewa katika hatua ya nusu fainali.
Wakicheza mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia juzi kati ya Zesco na Mufulira Wanderers ambao ulirushwa na Kituo cha SuperSport, mtangazaji wa mchezo huo alisema kuwa kiungo huyo anakwenda Simba kwenye usajili huu.
“Huyu anatakiwa na Simba ambayo ni kati ya timu kubwa za Tanzania, anaweza kwenda kwenye timu hiyo,” alisema mtangazaji huyo wakati mchezo ukiendelea.
Hata hivyo, mchezaji huyo amekuwa akitajwa mara kwa mara kuwa anaweza kujiunga na Yanga kwenye dirisha hili la usajili baada ya kocha wake, George Lwandamina kujiunga na timu hiyo ya Jangwani.
Hata hivyo, akizungumza na Championi Jumatano, mchezaji huyo amesema bado hajazungumza na Simba wala Yanga, lakini yupo tayari kutua kwenye timu yoyote.
“Sijazungumza na timu yoyote ya Tanzania, lakini kama watakuja Simba au Yanga nitajiunga nao, suala la msingi ni wenyewe kufuata utaratibu kwa kuwa bado nina mkataba na Zesco,” alisema Chaila.
Powered by Blogger.