KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Simba iliyokutana Novemba 18, Dar es Salaam, imeitisha mkutano maalum kwa ajili ya mabadiliko ya katiba

KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Simba iliyokutana Novemba 18, Dar es Salaam, imeitisha mkutano maalum kwa ajili ya mabadiliko ya katiba utakaofanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam.Taarifa ya Simba kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa mkutano huo utafanyika Desemba 11, mwaka huu katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

“Kamati ya utendaji imetumia mamlaka iliyopewa na Katiba ya Simba ibara ya 22 kifungu cha kwanza,” ilieleza taarifa hiyo jana na kuongeza:

“Nyaraka zote muhimu za mkutano huo zitakabidhiwa kwa wanachama kupitia matawi yao kwa mujibu wa matakwa ya katiba ibara ya 22 kifungu cha nne cha katiba ya klabu,” ilieleza.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa maazimio ya mkutano mkuu wa kawaida uliofanyika Julai 31, mwaka huu, ambao uliazimia kubadili mfumo wa uendeshwaji wa klabu na kuingia wa kuuza hisa.

Na kwa ujumla wanachama waliafiki mpango wa kumuuzia mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji asilimia 51 ya hisa kwa Sh. bilioni 20

Hata hivyo, serikali iliingilia kati mpango huo kwa kumshauri Mo Dewji na mfanyabiashara mwenzake anayetaka kukodishwa Klabu ya Yanga kwa miaka kumi kuanzisha timu zao kama mfanyabishara mwenzao, Said Salim Bakhresa kuliko kuzing'ang'ania klabu hizo.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja aliagiza kwanza kusitishwa michakato yote inayoendelea ya kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa wanachama kwenda katika umiliki wa hisa na ukodishwaji kwa Klabu za Simba na Yanga hadi kutakapofanyika marekebisho ya katiba zao.

Alisema klabu hizo zinapaswa kurekebisha katiba zao kwanza kabla ya kufanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442, kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9).
Powered by Blogger.