Hizi ni sababu inazofanya makampuni makubwa ya teknolojia kununua makampuni madogo/yanayochipukia

WhatsApp yanunuliwa kwa dola za kimarekani bilioni 19’, ’Facebook yainunua Instagram kwa shillingi za kitanzania trillioni…’ ni miongoni mwa vichwa vya habari ambavyo si vigeni sana kwenye macho yetu, kampuni fulani kununua kampuni nyingine.
facebook-whatsapp-buy-buyout
Ni jambo la kawaida kwenye ulimwengu wa teknolojia lakini unajua sababu kuu zinachofanya kampuni hizi kumwaga mabilioni ya pesa zote hizo? (Tena kwenye Apps zinazopatikana BUREE kwenye app stores?!Natania kidogo) kaa hapa nikujuze:-
Kuinua thamani ya hisa na uwekezaji
Kampuni kama Microsoft,Google,Apple zimejiandikisha kwenye masoko makubwa ya hisa duniani kama NASDAQ na moja ya sifa kuu ya kuwa na uwekezaji wenye thamani na unaoongezeka ni kuwa na huduma au bidhaa zenye mvuto kwa watumiaji muda wote,hivyo basi kampuni hizi kubwa hupenda kuwahi bidhaa au huduma mpya zinazoelekea kukua kwa kasi ili kuvutia wawekezaji wao na wawekezaji wapya jambo ambalo huinua kwa kiasi kikubwa thamani ya hisa za kampuni husika,ndio maana kampuni hizi muda wote huwa macho kodo kuangalia kampuni mpya/zinazochipukia zinazoweza kukidhi matakwa yao na kuwapatia faida katika masoko hisa.

Taarifa za watumiaji

Kila kampuni ina mfumo wake na sheria katika kukusanya na kutumia taarifa mbalimbali za watumiaji wake(Mfano,namba za simu,barua pepe anwani makazi n.k)na kutokana na hilo haiwezekani kampuni moja kuazima au kuchukua taarifa za watumiaji wa kampuni nyingine bila watumiaji wenyewe kuhamisha,lakini vipi kama kampuni hizi zikiwa chini ya mmiliki mmoja? Hilo linawezekana na kufanyika kwa urahisi zaidi na ndio maana baada ya Facebook kununua WhatsApp walirekebisha sheria zao za taarifa za wateja na kuwapa mamlaka Facebook kutumia anwani za wateja wa WhatsApp na marafiki zao moja kwa moja.
Taarifa hizi ni muhimu sana sababu ndizo hutumika katika mambo mbalimbali kama uonyeshaji wa matangazo, habari na taarifa mbalimbali kwa mtumiaji. Pia taarifa hizi hurahisisha kujiunga kwa huduma fulani kupitia taarifa zilizokwisha tolewa kwa huduma nyingine(Kama kujiunga YouTube au kutumia Firebase kwa kutumia taarifa za akaunti ya Google moja kwa moja bila kuidhinisha)Au jinsi Google wanavyotumia taarifa zako ulizoweka kwenye kifaa chako cha android moja kwa moja katika ushawishi wa matangazo na uwasilishaji wa taarifa mbalimbali.
Kubadilishana mifumo teknologia (API)
Kipindi cha nyuma kabla Instagram haijanunuliwa na Facebook, picha zilizowekwa instagram zilionekana kama link zikiwa shared Facebook, hii ni kwasababu kushea mifumo teknolojia (API) kuna mipaka yake, lakini daraja hili linaweza kuvukwa kama kampuni hizi zikifanya kazi pamoja na kuwa na uwezo zaidi ya unaoruhusiwa na API, ndio maana baada ya Facebook na Instagram kuwa kampuni moja picha za Instagram zinaonekana moja kwa moja Facebook endapo tu mtumiaji akitaka (Share)
Pia, ubadilishanaji mifumo huo ndio unaofanya iwezekane kulipia, kuandaa na kuangalia maendeleo ya matangazo ya Instagram kwa kupitia akaunti ya Facebook ya muhusika au kualika marafiki wa Facebook katika group la WhatsApp kupitia link moja kwa moja.

Kuendana na mabadiliko

Teknolojia kwa kiasi fulani ni kama fasheni, sababu vyote hubadilika badilika na hubadilika bila utabiri wa kitu gani kitakuwa na uhitaji zaidi.Hivyo inapotokea App fulani kutokea kupendwa na watumiaji huonekana kama bakuli la dhahabu, Instagram ilianzisha huduma ya video za sekunde kadhaa mwaka 2013 na ikaonekana ni kitu kipya sana na kuvutia, lakini huduma kama hiyo imekuwa ikitolewa na App ya Vine toka mwaka 2012 na kuonekana kawaida tu!
Periscope iliyoanzishwa 2015 ni App maarufu sana ya video za moja kwa moja lakini huduma kama hiyo imekuwa ikitolewa na Ustream, iliyokuwepo toka mwaka 2007!
Ubadilikaji huu na kutotabirika ndio unaofanya kampuni inayoonekana kupendwa kutafutwa sana na kampuni kubwa maana uanzishwaji wa huduma mpya kwa kampuni kubwa haumaanishi kufanikiwa kwake,hivyo ni bora kununua kitu ambacho tayari watu wameonyesha kuvutiwa nacho tofauti na kuiga na kukosa watumiaji wa kutosha.
Kukuza bidhaa/huduma
Android ni mfumo wa simu unaoongoza kwa umaarufu duniani ukifuatiwa na iOS, lakini pengine usingekuwa katika nafasi hiyo au ingechukua muda mrefu pasipo Google kununua mfumo huu mwaka 2005, sababu ya jina na uwezo wa Google, wingi wa wataalam iliyonayo imewezesha mfumo huu kuwa thabiti na wenye ushindani zaidi kwa iOS kuzidi hata mifumo iliyokuwa na nguvu kabla yake kama BlackBerryOS ya BlackBerry na Symbian ya Nokia zilizokuja kufa sababu ya ushindani mkubwa.
Uwekezaji huu wa Google ndio uliofanya Android kuwa na uwezo wa kutoa matoleo mapya kila mwaka na mabadiliko madogo madogo mara kwa mara kutokana na ushindani wa iOS wanaofanya hivyo pia, na ndio uliosaidia ushawishi kwa makampuni makubwa ya vifaa vya umeme kama Samsung na mengineyo kuwaamini na kufanya mfumo huo kuwa wa lazima kwa vifaa vyao na kuufanya pia uwe utanuke kutoka kwenye matumizi ya simu pekee mpaka kwenye vifaa vingine kama saa za mkononi na vifaa vya nyumbani kama jokofu, runinga na mashine za kufulia.
Utaalamu
Aliyekutangulia amekutangulia tu, kampuni kubwa zina uzoefu, wataalamu, miundombinu ya kutosha. Sababu ya ukubwa waliyonayo unazofanya wawe na wataalamu wa hali ya juu wanaolipwa pesa ya kutosha.
Hivyo kununua kampuni ndogo waliyovutiwa nao huwa ni ahueni fulani kwa kampuni hiyo kulingana na malengo yake ya kukua au kuongeza watumiaji, utaalamu huu husaidia katika kuboresha huduma za kampuni, kuongeza watumiaji na masoko pamoja na huduma nyingine, kampuni ya Firebase inayojihusisha na uhifadhi database iliyoanzishwa mwaka 2011 mpaka kufikia mwaka 2014 ilikuwa na watumiaji 110,000 lakini mwaka mmoja na nusu baada ya kununuliwa na Google ilipanda na kuwa na watumiaji zaidi ya 450,000!
Hivyo kwa kampuni yenye malengo ya ukuaji wa haraka kununuliwa na kampuni kubwa huwa ni jambo la neema.Pia utaalamu huu husaidia kupanua teknolojia husika katika kuwezesha kutumika katika mifumo tofauti na mazingira mbalimbali kutokana na ushawishi na nguvu ya kampuni mama.
Fedha/vipande
Pengine hili ndio jambo ambalo huzingatiwa sana wakati wa manunuzi haya, sababu kwanza…inaposemekana kampuni imenunuliwa sio kwamba imechukuliwa moja kwa moja toka kwa waanzilishi! Manunuzi ya kampuni yanahusisha uhamishaji wa teknolojia, taarifa na mfumo mzima wa wafanyakazi na utendaji toka kampuni inayonunuliwa kwenda kampuni nunuzi,ikimaanisha kwamba maamuzi makuu kuhusu bidhaa/huduma hiyo yatatoka katika kampuni mama lakini waanzilishi wa kampuni inayonunuliwa hupewa kiasi fulani cha pesa kutokanan na maelewano na thamani ya huduma/bidhaa husika pamoja na uwekezaji wa vipande hisa katika kampuni mama, hii ni katika kuhakikisha kuwa hata kama huduma/bidhaa iliyofanya kampuni kununuliwa ikiisha thamani au ikikosa watumiaji waanzilishi bado watakuwa wana hisa katika kampuni mama pamoja na uwezo wa kutoa maamuzi katika bodi kuhusu huduma/bidhaa nyingine na pia kuendelea kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Kuwa na bidhaa ya tofauti
App inapokua kwa kasi na kupata wateja wengi hujipanga kwa ajili ya kupata faida kutokana na mtaji mkubwa wa watumiaji wake, lakini ili kuwa na uhakika zaidi na kujihakikishia wateja wa aina tofauti tofauti huitaji kuwa na huduma yenye utofauti kidogo na bidhaa/huduma yake iliyozoeleka kuliko kujiweka kwenye box la huduma/bidhaa moja.
Ndio maana kampuni kama Snapchat iliamua kununua kampuni inayochipukia ya Spectacles inayojihusisha na utengenezaji wa miwani zenye uwezo wa kupiga picha sababu Snapchat kama kampuni inajiandaa kuingia kwenye soko la hisa(IPO) hivyo lazima ijitanue tofauti na huduma ya application za simu pekee ambayo pengine inafanya itumike sana na tabaka la aina moja sana kuliko matabaka mengine(Vijana) na ununuzi huo kupanua wigo na tabaka la watumiaji na huduma, sababu watumiaji wa spectacles kabla haijanunuliwa watahama na ununuzi huo hivyo Snapchat kuongeza mtaji wa watumiaji na utanuzi wa huduma zake.
Uzoefu
Mwisho wa yote hii ndio sababu kuu inayofanya kampuni kubwa kuwa na kiburi na uwezo wa kununua kampuni changa/zinazochipukia, hapa nazungumzia uzoefu katika nyanja zote za kiteknolojia, biashara, mawasiliano, ujuzi na kila kitu kuhusu huduma na hali ya soko.
Kampuni iliyokuwa na muda mrefu kwenye soko ina uzoefu wa kutosha kuhusu bidhaa/huduma pamoja na mambo mengine kadha wa kadha ambayo kampuni ndogo hukosa na hivyo kutoa mwanya wa kununuliwa ili kulinda ukuaji wake,mfano kampuni ya kutengeneza michezo ya simu ya King yenye michezo maarufu kama Candy Crash Saga,Pet Rescue Saga na mengineyo,baada ya kupata faida ya kutosha kutokana na mauzo ya michezo hiyo iliamua kuingia kwenye soko la hisa kwa kuweka vipande vyake hadharani(IPO)
Lakini kinyume na utabiri wa thamani, ununuzi halisi ulikuwa sio wa kuridhisha na sababu kubwa ni wanunuzi na wawekezaji wengi kutokuwa na imani kwamba kampuni hiyo ingeendelea kupata faida kwa muda mrefu na kwa kutegemea huduma moja tu ya michezo pekee tena inayofanana ,jambo ambalo pengine lingeepukika kama King wangekubali kununuliwa mapema waingie kwenye soko chini ya mwamvuli wa wazoefu,uwekezaji ungekuwa maradufu na faida ingeongezeka somo lililokuja kuwaingia baadae sana na kuwafanya wakukubali kununuliwa Februari 2016 na Activision ambao ni maarufu na wazoefu wa miaka mingi kwenye kutengeneza michezo mbalimbali ya kompyuta.
Baraka W. Mgalula
Twitter: Barker5lime
Twitter.com/Barker5lime
Powered by Blogger.