DHAHABU KWENYE PUA YA NGURUWE

Awali sikuwa nafahamu hasa, nini ilikuwa maana ya mtunzi wa msemo “Mwanamke mrembo asiye na akili ni sawa na pete ya dhahabu kwenye pua ya nguruwe.” Iliniwia vigumu sana kuelewa nini kilikuwa kimefichwa nyuma ya ujumbe wa huyu bwana. Kweli fumbo, mfumbie mjinga…

Dunia haikutokea mwanamke mbaya ingawa urembo wao na maumbo yao yanatofautiana kiasi Fulani. Kwetu sisi wavaa suruali ambao tunajiita wanaume tumekuwa washabiki wakubwa wa wanawake ambao kwa makusudi kabisa tukaamua kuwabatiza jina Warembo. Jina hili bila shaka ni matokeo ya kile kinachoshuhudiwa na mboni za macho yetu. Macho bwana, eti yamekuwa mashuhuri kutushuhudia na kuushawishi moyo uamini kile ambacho yenyewe yanakiona (Urembo wa mwanamke). Laini huwa nayaonea huruma sana macho pale ambapo yanapogonga mwamba na kushindwa kutambua urembo ama ubaya uliojificha kwa ndani. Macho mpaka leo hii yameshindwa kuona, ama kutambua haiba iliyohifadhiwa ndani ya maumbo na sura nzuri ya huyu mwanamke tuliyeamua kumwita mrembo.

Hapa sasa nikaanza kupata kijimwanga juu ya kauli ya huyu bwana. Hebu kwa pamoja tumwangalie mwanamke huyu ambaye sasa urembo wake unafananishwa na pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe. Najaribu kumjengea picha mwanamke ambaye huyu bwana alimwita mrembo, ni hakika hakuwa na mashaka katika kauli yake. Bila shaka alikuwa na urembo na mwenye kuvutia kiasi cha kuweza kuiteka akili ya mwanaume yoyote mkwale. Kiukweli alikuwa ni dhahabu ing’aayo tena katika jua la utosi ambayo kama utaiangalia bila tahadhali basi miyale yake isingesita kukutia upofu wa maisha.

Namfananisha mrembo huyo wa miaka hiyo, na mrembo ambaye ametokea wa aina ile ile katika karne hii mpya ya Sayansi na Teknolojia. Pengine wanaweza kuwa na tofati kidogo lakini sidhani kama zinaweza kuwafanya watofautiane kwa kiasi kikubwa. Karne hii, nchi Tanzania amepata kutokea mwanamke JUHA ambaye urembo wake uliyavutia macho ya ndugu yetu ambaye kwa sasa ni Mbunge. Ni wazi Mbunge huyu ambaye awali alikuwa msanii mkubwa kabla ya kujiingiza katika siasa alivutiwa na dhahabu hii.

Lakini masikini urembo wake wa nje, utanashati wake wa nje, mvuto wake wa nje vyote hivyo vimeshindwa kumsaidia. Wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi, sidhani kama kuna mwanamke ambaye anaujua uchungu wa mwana hasa angediriki kukifanya alichokifanya mwanamke huyu ambaye nina mashaka na akili yake. Mwanamke ambaye anadiriki kurekodi video ambayo inamdhalilisha mwanae na kuipost katika mitandao ya kijamii. Ni kweli nina uelewe mdogo sana lakini hili halihitaji eliimu ya chuo kikuu kulipambanua. Kila mtu anajua kuna sharia chungunzima ambazo watunzi wake aliyaona haya ambayo baadhi yetu tunayapitia kwa namna moja au nyingine. Sheria ambayo kazi yake ni kuwashurutisha wale wanaokwepa kutekeleza majukumu yao kwa makusudi.

Ananishangaza mwanamke huyu ambaye ameamua kuifanya Instagram kuwa balaza lake la wazee ambalo anatarajia utatuzi wa swala lake. Ama ameifanya Instagram ni ukumbi wa mahakama ambao una sikiliza mashitaka ya watu na kuamua haki. Na kama ulikuwa unataka kuishitakia Instagram na kuueleza ulimwengu kuhusu huyo mwenzio kwanini hukujirekodi mwenye hiyo video yako na kuipost? Kwanini ukifanyie kiumbe kisicho na hatia? Hatia yake ni kuzaliwa na wewe? Mzazi yoyote mwenye akili timamu hawezi kufanya kitu ambacho kimefanywa na huyu mwanamke. Sasa namuelewe yule aliyepata kusema, mwanamke yoyote anaweza kuzaa, lakini wenye uwezo wa kuwa mama ni wachache.
Powered by Blogger.