Simba Sc: Hatutaki kudondosha hata pointi moja

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara
ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE mjini Dar es Salaam kwamba,
japokuwa Mbao FC imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini hawataidharau.
“Hatupaswi kubweteka kwa matokeo mazuri ya sasa, tunatakiwa tuendelee
kufanya vizuri, tusipoteze hata pointi moja. Hatutaki hata droo, lazima
tushinde kila mechi, ili tuendelee kuwaacha washindani wetu katika mbio
za ubingwa (Azam na Yanga),”alisema.
Hajji amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi leo Uwanja wa
Uhuru kuisapoti timu yao ikimenyana na Mbao inayocheza Ligi Kuu kwa mara
ya kwanza msimu huu kihistoria.
Simba SC ambayo imeweka kambi Ndege Beach Hotel, Mbweni, Dar es Salaam,
ikijifua Uwanja wa Boko Veterani, itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na
kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar
mabao 2-0 Uwanja huo huo wa Uhuru.
Simba SC inagongoza Ligi Kuu sasa ikiwa imejikusanyia pointi 23 baada ya
kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Stand United ya Shinyanga yenye
pointi 20 za mechi 10, wakati mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 18
za mechi tisa ni ya tatu.