Mchezaji Chirwa atoa gundu, aanza kutupia mabao Yanga

Hatimaye mshambuliaji wa Kimataifa wa Yanga kutoka nchini Zambia Obrey Chirwa leo amefunga goli lake la kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo msimu huu.
Chirwa ameifungia Yanga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa leo katika dimba la Uhuru Dar es Salaam.
Mabao mengine ya Yanga katika mchezo huo yamefungwa na Donald Ngoma na Simon Msuva huku Haruna Chanongo akiifungia Mtibwa bao la kufutia machozi.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, vinara Simba wanaendelea ubabe kwa Mbeya City baada ya kuichapa mabao 2-0 katika dimba la Sokoine Jijini Mbeya.
Mabao ya Simba yamefungwa Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya huku Fredrick Blagnon akipoteza penati iliyopangiliwa na kipa wa Mbeya City.
Katika mchezo huo Mrundi Laudit Mavugo aliwekwa bench huku Blagnon, Ajibu na Kichuya wakianza katika safu ya ushambuliaji ya Simba.
Katika mchezo mwingine matajiri wa Chamazi wamekutana na moto mwingine baada ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United katika mchezo uliopigwa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Jijini Mwanza Mbao FC imeiadhibu Toto Africans mabao 3-1 huku Majimaji ikipoteza tena nyumbani kwa kufungwa na Kagera Sugar bao 1-0.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaoikutanisha Ruvu Shooting dhidi ya Ndanda FC katika uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Powered by Blogger.