Mbao Fc sasa inamdai Mbunge wa CCM laki 6 za magoli waliyofunga



WAZIRI ANGELINA MABULA

Timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza, jana ilishuka uwanjani kukipiga dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kupata ushindi pamoja na kuongeza pato lao kutoka kwa waziri ambaye pia ni mbunge.
Mbao FC inayoshiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza iliahidiwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa atanunua kila bao watakalofunga kwenye ligi hiyo kwa shilingi 50,000.
Katibu Mkuu wa Mbao FC, Richard Athanas, amesema kuwa kabla ya mchezo wa jana, ahadi yao kutoka kwa kiongozi huyo aliye chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ilikuwa imefika shilingi 600,000 kutokana na mabao waliyofunga. 
“Waziri Mabula alituahidi kuwa atakuwa ananunua kila bao letu tutakalokuwa tunafunga katika mechi zetu za ligi kuu kwa shilingi 50,000, lengo likiwa ni kutoa hamasa kwa timu yetu kufanya vizuri kwa sababu inatoka jimboni kwake.
“Mpaka sasa tumeshafunga mabao 12 katika mechi zote tulizocheza, hivyo ukiyazidisha mara 50,000 utaona kuwa tunamdai kiongozi wetu shilingi laki sita.
“Hatuna wasiwasi naye kwani tunaamini atatupatia muda wowote fedha hizo, lakini pia vijana wetu kwa upande mwingine wanaendelea kupambana kuongeza mabao ili kitita hicho kizidi kuongezeka,” alisema Athanas.
SOURCE: CHAMPIONI
Powered by Blogger.