Makamba atoa siku 5 kusitishwa shughuli hizi Ziwa Rukwa

Waziri wa Mazingira na Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe January Makamba  amesema serikali itatangaza eneo la Ziwa Rukwa kuwa eneo nyeti la Mazingira ambapo ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote za Kilimo na Ufugaji zinazofanyika katika kingo za Ziwa Rukwa na kutoa siku 5 hadi tarehe 28 mwezi huu kuhakikisha agizo hilo limetekelezwa.
Makamba ametoa tamko hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nankanga, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa  eneo la Forodhani lililopo katika fukwe za Ziwa Rukwa kufuatia ripoti ya kina cha Ziwa hilo kupungua kwa takribani mita 3 katika kipindi cha miaka 16 ambapo mwaka 2000 kina hicho kilikuwa mita 6 na hivi sasa ni takribani mita 3 pekee.
Katika kulinusuru Ziwa hilo Waziri Makamba ameagiza kuwa kuanzia tarehe 28 ya mwezi huu haitoruhusiwa kufanya Kilimo ndani ya Mita 60 za ukingo wa Ziwa kama inavyotakiwa na Sheria ya Mazingira, Sheria ya Maji na Sheria ndogo za Serikali za Mitaa lakini vilevile kuanzia tarehe 28 mwezi huu haitoruhusiwa kuchunga na kufuga mifugo ndani ya mita 200 za ukingo wa Ziwa.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema Serikali itatoa agizo kwa Halmashauri zote za Wilaya ambazo Ziwa Rukwa linapita kukutana na kukusanya pesa kutoka katika vyanzo vyake ili ziweke alama (Beacon) na vibao katika mita 60 na Mita 200 kutoka kwenye Ziwa kujulisha umma kuwa hairuhusiwi kufanya shughuli katika maeneo husika.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake mahsusi ya mazingira katika Mikoa 10 ambapo amepokea taarifa ya Halmashauri ya Mazingira na Misitu ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo mbali na mengine imeonesha kuwa imeshatoa notisi kwa wavuvi wanaotumia  zana haramu kwa uvuvi kuzisalimisha zana hizo kwa hiari hadi Novemba 17 na baada ya hapo mamlaka husika na vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki
Powered by Blogger.