responsive ads

Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa jumla ya askari wake wanne wameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya majambazi kuvamia tawi la benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

14021451_1204196806310978_8100559727598590904_n
Akizungumza moja kwa moja kupitia kituo cha Redio One Stereo leo asubuhi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema watu kadhaa wamekatawa na msako unaendelea ili kuwapata waliotekeleza unyama huo.
Sirro amesema taarifa kutoka eneo la tukio zinaonesha kuwa majambazi hao walikuwa 14 na baada ya kufanya mauaji hao, walivamia kituo cha polisi cha Mbande kisha wakavunja stoo na kuchukua sare ya askari na silaha.
Akielezea namna tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Sirro amesema wahalifu hao walitumia mwanya wakati askari wakibadilishana lindo katika taasisi hiyo ya fedha na kuibuka ghafla na kuanza kurusha risasi.
Kwa mujibu wa Sirro, gari la polisi limechakazwa kwa risasi na askari mmoja aliyekuwa lindo alifanikiwa kukimbia na ndiye aliyeweza kutoa taarifa na maelezo ya namna tukio lilivyofanyika.
“Watu kadhaa wamekamatwa na tunaendelea na msako. Tunawataka wakiwa hai au wafu,” amesema Kamanda Sirro huku akiwataka watu kujihadhari na yeyote anayejitambulisha kwao kuwa ni askari bila kuonesha kitambulisho.
Ameendelea kusema kuwa baada ya operesheni ya kukomesha mtandao wa wahalifu kama hao na wengine kukimbilia nchi jirani, masalia wameanza kujikusanya na kutekeleza matukio ya mauaji huku askari wakilengwa.
Pia Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye na yeye alifika eneo la tukio usiku huo amesikitishwa na tukio hilo la kinyama.
“Usiku huu nimefika Mbande – Temeke, eneo lilipofanyika tukio baya la uhalifu wa kutumia silaha ambapo watu/majambazi zaidi ya saba wakiwa na silaha wamevamia eneo la Benki ya CRDB-Mbande na kuua askari 4 waliokuwa wakishuka kwenye gari tayari kwa kupokezana lindo,” aliandika Waziri kupitia instagram.
Aliongeza, “Pia wamejeruhi raia wa kawaida wawili, nimewajulia hali zao na wote wanaendelea vizuri. Hatutaishia kulaani tu tukio hili na matukio mengine kama haya, natoa rai kwa wahusika kujisalimisha. Vilevile Wananchi na raia wema tunaomba ushirikiano wenu katika vita hii ya kupambana na wahalifu hawa na wanaotuzunguka kwenye maeneo yetu,”

Source: Mwananchi/ Mitandao ya kijamii
middle 300x250
Powered by Blogger.